HABARI KUU:

GACHAGUA ALIYEMUITA RAILA MAJINA SASA AMMEZEA MATE 2027..//..LUSAKA AMKAUKIA SENETA ONYONKA KWA KUMUITA MPUMBAVU!..//..GEN Z WA BANGALADESH WAVAMIA IKULU YA WAZIRI MKUU..//..AJALI SACHANGWAN HUKU WANAFUNZI 25 NA WAALIMU 3 WAKIPATA MAJERAHA MABAYA..//..MGOMBEA urais wa Chama cha Democrat Kamala Harris amemteua Gavana wa Minnesota Tim Walz kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa urais wa Novemba 5, mwaka huu.// AMERIKA imeonya serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi kukabili waandamanaji na kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu..//GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza anataka Mahakama Kuu kuwahukumu maafisa wawili wa bunge la kaunti na MCA aliyeteuliwa kwa madai walidharau mahakama, akisema walipuuza maagizo ya korti kwa kukusudia kumtimua kwa mara ya tano.

Thursday, 15 August 2024

TRUMP AMPIGA KAMALA KWA MAMBO MAZITO HUKU UMAARUFU UKIENDELEA

 


MGOMBEAJI wa urais wa chama cha Republican, Donald Trump, Jumatano alishambulia sera za mpinzani wake wa chama cha Democratic, Kamala Harris, katika hotuba aliyotoa akiwa Asheville, North Carolina huku kura za maoni zikionyesha umaarufu wake unazidi kupungua.

Baadhi ya washirika, wafadhili, na washauri walionyesha wasiwasi kuhusu mashambulizi ya Trump kwa makamu huyo wa rais wa Amerika na kupendekeza alenge sera zilizofeli ambazo Harris alitetea akiwa afisini.

Akihutubia wafuasi wake, Trump aliepuka mashambulizi kuhusu rangi ya Harris na kuzamia sera zaidi kinyume na awali.

Lakini aliendelea kumtupia matusi ya kibinafsi, kwa kumuita mshenzi na kukejeli kicheko chake, akisema mpinzani wake ana shida kubwa.

Kujiondoa kwa Rais Joe Biden kwenye kinyang’anyiro cha urais Novemba 5 na kumuidhinisha Harris, mwezi uliopita, kulileta wimbi jipya katika kampeni.

Kura za maoni zinaonyesha Harris anaziba pengo la umaarufu dhidi ya Trump. Baadhi ya kura hizo zinaonyesha Harris yuko mbele katika kinyang’anyiro hicho cha Novemba 5.

Ujio wa Harris ulivuruga kampeni ya Trump, ambaye awali alitumia matusi huku akimlenga Makamu wa Rais ambaye mama yake alizaliwa India na baba yake Jamaica.

Trump alisema kuwa ataidhinisha hivyo basi kurahisisha mchakato wa kutoa vibali vya uchimbaji mafuta pamoja na kupunguza bei iwapo atamshinda Harris.

Pia aliahidi kupunguza bei za nishati na umeme kwa nusu, ndani ya miezi 12 hadi 18, baada ya kuingila mamlakani.

Hakubainisha wazi jinsi atakavyofanya hivyo, lakini alirudia ahadi za awali za kuongeza uzalishaji wa mafuta, ikiwemo katika Hifadhi ya Kitaifa ya Wanyamapori ya Artic, Alaska, ambapo utawala wa Biden ulisitisha utoaji wa vibali vipya.

Alimshutumu Harris kwa kuunga mkono marufuku ya kuchimba mafuta kwa kutumia teknolojia mwaka wa 2019 akisema msimamo wake utakuwa tatizo kubwa katika jimbo muhimu la Pennsylvania.

Kabla ya mkutano wa Trump huko Asheville, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampeni ya Harris, Michael Tyler, alituma taarifa akimshutumu Trump kwa kupuuza tabaka la kati kwa kupinga ulinzi wa vyama vya wafanyakazi na kuunga mkono kupunguzwa kwa ushuru wa makampuni.

Tyler alisema Harris atafanya ziara yake North Carolina, atakapozungumzia sera za kiuchumi katika hotuba yake huko Raleigh.

“Ataeleza mpango wa kupunguza gharama kwa familia za tabaka la kati na atakavyoshughulikia ushuru wa makampuni,” alisema Tyler.

Sunday, 11 August 2024

HUENDA MATIANG'I AKAWA RAIS 2027 BAADA YA RUTO KUKOSA UMAARUFU

 

Aliyekuwa waziri zamani fred matiangi anayetaka urais
2027 

ULINGO wa siasa nchini huenda ukabadilika pakubwa iwapo aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani, Dkt Fred Matiang’i, atajibwaga katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Yamkini kutakuwa na mazingira mapya ya kisiasa iwapo Dkt Matiang’i atadumisha uungwaji mkono ambao vijana wanaashiria kumpa.

Duru zinasema kwamba Dkt Matiangi ameanza kujiandaa  kugombea urais kwa kuajiri kampuni ya kimataifa kusuka mikakati ya kufanikisha azma yake.

Wadadisi wa kisiasa wanasema kuna uwezekano atakuwa mwanasiasa anayemezewa mate na wagombeaji wengine wakitaka aungane nao.

Waziri huyo wa zamani anatambuliwa kwa misimamo yake mikali na maamuzi thabiti katika wizara tatu alizosimamia chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.

 Japo amekuwa kimya, jina lake liliibuka katika kilele cha maandamano ya vijana kulalamikia gharama ya maisha na ufisadi serikali.

 Maandamano hayo yalipokuwa yakichacha, jina la Dkt Matiang’i,  ambaye  inasemekana anaishi ng’ambo liliibuka baadhi ya watumiaji wa mitandao wakimtaka  kujitokeza ili kujiunga nao kupigania uongozi bora na hata Rais wa Kenya 2027.

Vijana hao walisema kuwa Dkt Matiang’i alikuwa kiongozi aliyefanikiwa katika wizara mbalimbali alizosimamia.

“Matiang’i, mambo ni mawili: ujitokeze ama tuje tukuchukue. Tunahitaji uwe rais na si tafadhali,” Naomi Waithira aliandika kwenye mtandao wa X.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, iwapo umaarufu wake miongoni mwa vijana utadumu, Dkt Matiangi atakuwa mwanasiasa mwenye thamani kubwa katika uchaguzi mkuu ujao ikizingatiwa mikakati anayosemekana kutumia kujijenga na kujipigia debe.

 “Wanaofahamu mikakati ya siasa watakwambia kuwa jina la Dkt Matiang’i halikuibuka kwa bahati wakati  wa  kilele cha maandamano. Ni mkakati wa kutumia matukio yanayofuatiliwa na watu wengi kuwasilisha ujumbe ili ufikie watu wengi,” akasema mdadasi wa siasa Kephar Miruka.

“Akitumia mikakati kama hii bila kuchoka, na ikizingatiwa ushawishi na utendakazi  wake akiwa waziri ulioacha alama chanya  kwa Wakenya, basi atakuwa kama mwanamwali spesheli atakayewaniwa na wanasiasa wakitaka waungane naye katika uchaguzi mkuu wa 2027.”

Kulingana na mchambuzi huyu, Dkt Matiangi anaweza kunyima vigogo wa miaka mingi wa siasa kura za vijana kote nchini na za kaunti za Kisii na Nyamira na kuwa mfalme kivyake.

optimizelegibility; vertical-align: baseline;">Hii ni ikizingatiwa kuwa viongozi wa mashinani katika kaunti hizo  wanamuunga mkono.

Rais William Ruto atatetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Kufikia sasa, ni kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye ametangaza azma ya kumpinga Rais Ruto.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga anagombea uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika ambao akishinda hataweza kugombea urais katika uchaguzi wa humu nchini.

Mwezi jana kakake, John Matiang’i alisema kuwa waziri huyo wa zamani  anafuatilia matukio ya siasa nchini.

 Bw  Miruka anasema  kwamba hata kabla ya maandamano ya vijana wa Gen Z dhidi ya serikali kuibuka, jina la Dkt Matiang’i lilikuwa vinywani mwa Wakenya.

“Anapendwa na Wakenya na zaidi ya yote na vijana ambao ndio idadi kubwa ya wapiga kura na wasio na ukabila. Hii pekee inakuonyesha kuwa ni mtu anayeungwa mkono na idadi kubwa ya wapiga kura na huyo ni mtu ambaye anaweza kuwatia tumbojoto wapinzani wake,” akasema.

Magavana Amos Nyaribo (Nyamira) na Simba Arati (Kisii), wamekuwa wakipigia debe kurejea kwa Dkt Matiang’i kwenye ulingo wa kisiasa.

“Tulikuwa na mtu wetu, Dkt Matiang’i, ninajua atakuja wakati unaofaa. Tutakuwa naye. Tuna viongozi wengine ambao watajibwaga uwanjani 2027. Tumedhamiria kuhakikisha kuwa siku moja, Omogusii (mtu wa jamii ya Abagusii) atakuwa kiongozi wa nchi,” akasema Bw Arati.

Wadadisi wanasema Matiang’i ana mtandao mkubwa wa marafiki aliounda akiwa waziri wa usalama wa ndani na ushirikishi wa serikali ya kitaifa ambao unaweza kufanya kupangua mikakati ya wagombeaji wengine wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Ninachojua ni kwamba atamezea mate sana na viongozi wengine na vyama vya kisiasa  wakitaka ndoa ya kisiasa,” akasema mchambuzi  wa siasa Dkt Isaac Gichuki.


KANISA KUFAIDI KWA KSHS.23MILIONI KWA KUUZIWA SHAMBA HEWA


 MAHAKAMA ya Mazingira na Ardhi imetoa uamuzi ambapo mwanamke mmoja anatakiwa kulipa kanisa la Katoliki Dayosisi ya Nakuru Sh23 Milioni.  

Sasa mwanamke huyo anatakiwa kurejesha pesa alizopokea kwa njia ya ulaghai baada ya kushtakiwa kwa kuuzia kanisa ardhi hewa.

Jaji Anthony Ombwayo alimwagiza Bi Hannah Wairimu Kahiga alipe pesa hizo zinazojumuisha Sh 19,800,000 ambazo kanisa lililipa kwa ununuzi wa shamba la ekari 11 katika eneo la Kiambogo, kaunti ndogo ya Naivasha na Sh 3, 960,000 kama fidia.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya kubainika kuwa mshtakiwa aliuza shamba la mtu mwingine kwa kutumia hati bandia.

Bi Hannah Wairimu anadaiwa kushirikiana na maafisa katika afisi ya ardhi kuuza shamba hilo la ekari 11 ambalo ni sehemu ya shamba la Teresia Wanjiru Wangera aliyefariki 1981.

“Mshtakiwa wa Kwanza (Bi Wairimu) hajathibitisha kwa mahakama hii kwamba alipata hatimiliki kihalali na kiutaratibu alipouza mali hiyo kwa Mlalamishi (Kanisa Katoliki),” Jaji Ombwayo akaamua.

Kanisa kupitia wadhamini wake waliosajiliwa ambao maafisa wao wa sasa ni Maurice Muhatia, Askofu Mkuu Kisumu, baba Lawrence Mbogo na baba Simon Kamau walimwendea Bi Wairimu kwa nia ya kununua ardhi hiyo kwa mradi wa kanisa.

Thursday, 8 August 2024

"WACHANA NA WAANDAMANAJI" AMERIKA YAONYA KENYA



 AMERIKA imeonya serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi kukabili waandamanaji na kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Waziri msaidizi wa Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Kibinadamu wa Amerika aliyezuru nchini Uzra Zeya ameelezea wasiwasi mkubwa wa nchi yake kuhusu ukatili wa polisi wa Kenya, akisema ni ukiukaji wa Katiba ya Kenya ya 2010.

Mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili nchini Kenya, Bi Zeya ameitaka Kenya ijitolee kuzingatia sheria na kuheshimu haki za binadamu, kuchunguza visa vya kutoweka, utekaji nyara na kukamatwa kiholela kwa waandamanaji.

Akiwahutubia wanahabari katika Ubalozi wa Amerika kabla ya kuondoka nchini, Bi Zeya alifichua kwamba alisisitiza umuhimu wa uhuru wa kujieleza, kukusanyika na uhuru wa vyombo vya habari ili demokrasia iweze kustawi.  Bi Zeya aliyasisitiza haya alipokutana na Rais William Ruto, mashirika ya serikali na maafisa wakuu serikalini.

Shutuma dhidi ya makosa ya serikali kwa raia

“Katika mazungumzo yangu na Rais Ruto na maafisa wakuu wa Kenya, nilishutumu ghasia zilizofanywa dhidi ya waandamanaji waliodumisha amani, watetezi wa haki za binadamu na wanahabari na nikahimiza kulindwa kwa uhuru wa kimsingi wa kukusanyika kwa amani na kujieleza, kama ilivyo katika Katiba ya Kenya,” alisema.

“Pia nilisisitiza umuhimu mkubwa wa vikosi vya usalama kujizuia, kujiepusha na ghasia za aina zote, na uchunguzi wa haraka na uwajibikaji kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi, na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu uliotekelezwa na polisi.”

Alisema kuwa ziara yake nchini Kenya ilijiri wakati nchi inakabiliwa na wakati mgumu kwa demokrasia hasa katika kukabiliana na maandamano yanayoongozwa na vijana  wakitaka utawala bora na kulalamikia ufisadi.

RUTO ALITUMIA NJAA YA RAILA

 


RAIS William Ruto alitumia azma ya uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kama mtego hadi akakubali chama chake kushirikiana na serikali kisiasa.

Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba Bw Raila hakufaulu kujinasua kwenye mtego wa Rais Ruto kwa kuwa anataka kuungwa mkono na serikali katika azma yake ya kugombea wadhifa huo wa Bara.

Kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua anasema Bw Odinga aliangukia mtego na hila za kisiasa alizowekewa kijanja na Rais Ruto.

Kulingana na Bi Karua, Bw Raila alijiondoa katika siasa za upinzani ili kuzingatia kampeni yake ya uenyekiti wa AUC ambayo anahitaji kuungwa mkono na serikali ya Kenya.

“Raila alijiondoa katika siasa za upinzani ili kufanya kampeni zake za kuwania kiti cha AU ambacho anahitaji Kenya Kwanza ndipo akipate.

Ni lazima apendekezwe na serikali ya Kenya na nadhani hapa ndipo mtego ulipomnasa na unaweza kuona wakati wa kuingia serikalini ni ule ambao stakabadhi zake ziliwasilishwa rasmi,” Bi Karua alisema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio hivi majuzi.

Kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, amejitangaza kuwa kiongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja-One Kenya huku Bw Raila akiendelea na kampeni zake za kugombea wadhifa wa Bara.

Bi Karua anasema kuwa Bw Raila hana budi kuunga serikali iwapo anataka azma yake ya kiti cha AU ifaulu.

Hapa, kulingana na Bi Karua, ndipo mtego ulipotegwa na Rais Ruto.

Katika tukio ambalo Rais Ruto alitaja kama serikali jumuishi, kiongozi huyo wa Azimio alitoa baadhi ya viongozi wa ODM kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri la serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Ruto aliteua manaibu viongozi wa ODM, Ali Hassan Joho, Wycliffe Oparanya, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi na mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho John Mbadi.

Bi Karua aliondoa chama chake katika muungano wa Azimio kufuatia hatua ya ODM kujiunga na serikali. Katika hafla zaidi ya moja, Bw Raila alikanusha makubaliano ya aina yoyote na Rais Ruto.

Hata hivyo, mnamo Jumatatu, waziri huyo mkuu wa zamani alipokuwa akizungumza katika Soko la Toi, Nairobi, alidai kuwa Rais Ruto aliomba msaada kutoka kwake ili kukomesha vuguvugu la Gen-Z ambalo lilikuwa likitishia kupindua serikali yake.

“Uliona wamelemewa na kazi, wakawafuta kazi waziri, wakaja kwetu wakiomba watu. Walikuja wakipiga magoti wakiomba tuwachangie baadhi ya watu,” Raila alifichua.

Kulingana na mchambuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki, Bw Raila alijipata katika mtego asioweza kujinasua kwa kutaka serikali iidhinishe azma yake ya kugombea uenyekiti wa AUC.

“Kile ambacho Bw Raila na Ruto hawawezi kukiri ni kwamba kila mmoja alihitaji mwingine. Raila alihitaji Ruto zaidi katika azma yake ya AUC naye Ruto alihitaji Raila amsaidie kuokoa serikali yake iliyotishiwa na maandamano ya vijana,” akasema.

Wednesday, 7 August 2024

MAGAVANA CHINI YA MWENYEKITI WAO WATISHIA KUZIMA NDOTO YA SHIF IWAPO MALIPO YA NHIF HAYATATIMIZWA

 

Ann Waiguru akiongea na wanahabari

MAGAVANA wanaitaka Wizara ya Afya kupatia kipaumbele malipo ya Sh8 bilioni ambazo Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Kitaifa (NHIF) inadaiwa na hospitali za kaunti kabla ya kuhamia katika Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF).

Miezi kadhaa baada ya hospitali za kibinafsi kote nchini kuondoa huduma zao kwa Wakenya walio na kadi za NHIF kutokana na deni lingine, ni hospitali za umma za kaunti pekee zinazokubali kadi za NHIF na kuwalazimu Wakenya kutoka jamii maskini kufurika katika hospitali za umma kusaka huduma za afya.

Magavana wameonya kuchelewesha kumaliza kulipa deni hilo kutawasababishia mateso zaidi Wakenya wenye mapato ya chini wanaotegemea huduma hizo.

Kaunti za Nairobi na Nakuru ni miongoni mwa zinazodai NHIF kiasi kikubwa cha pesa huku Nairobi ikidai kiasi kisichopungua Sh2.1 bilioni na Nakuru Sh540 milioni kutoka kwa NHIF na Linda Mama.

“Tunapohamia SHIF, hatutaki kuona hali ambapo Sh8 bilioni zinageuka kuwa malimbikizi ya deni ambalo halijalipwa kwa vituo vya afya. Tunataka NHIF ilipe vituo ambavyo madeni yake yangali hayajalipwa. Ni kwa namna hiyo tu tutaweza kuhamia SHIF bila deni lolote linalodaiwa na vituo vya kaunti,” Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Baraza la Magavana, Gavana Muthomi Njuki alisema Jumanne.

Gavana wa Nakuru, Bi Susan Kihika, alielezea wasiwasi wake, akisema Nakuru pekee inadai NHIF na mpango wa Linda Mama kitita cha Sh540 milioni.

“Hali ya kukosa kulipa ni mzigo mzito mno kwa hospitali zetu na huenda hivi karibuni ikalemaza oparesheni. Tunahimiza Wizara ya Afya kupatia kipaumbele deni kwa sababu hospitali zetu tayari zimeathirika vibaya na kucheleweshewa malipo. Jijini Nakuru, kwa mfano, tunaona bidhaa zinazozidi kuwasilishwa lakini tunabeba mzigo kwa sababu hatupati malipo,” alisema Gavana Kihika.

Wizara ya Afya (MoH) na Baraza la Magavana (CoG) linaloongozwa na Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, hapo mbeleni limekutana kujadili masuala yanayohusu madeni huku mchakato wa kuhamia SHIF ukiendelea.

Mikutano hiyo iliangazia masuala muhimu ambayo ni pamoja na madeni.

MoH na serikali za kaunti zimeafikiana vilevile kuendesha kampeni ya umma kuhusu usajili wa wanachama wanaojiunga na SHIF.

Pande hizo mbili zitaendelea kushirikiana ili kuhakikisha utekelezaji bora wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC).

Waliafikiana vilevile kuwa MoH itatumia mfumo na data inayotumika kwa sasa katika NHIF iliyovunjiliwa mbali, kabla ya kuzindua SHIF.

MAHAKAMA YAMWAGILIA MAJI BARIDI UWEZEKANO WA DCI KUWAKAMATA WANDANI WA GACHAGUA WANAOSHUKIWA KUPANGA MAANDAMANO YA GEN Z

 

Naibu Rais Gachagua kwenye picha    

MAHAKAMA Kuu imeamuru polisi wasiwatie nguvuni wabunge wawili wanaodaiwa kufadhili maandamano ya vijana yaliyopelekea watu zaidi ya 60 kuuawa na zaidi ya watu 600 kujeruhiwa.

Jaji Enock Chacha Mwita aliwaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin wasiwakamate Wabunge James Mwangi Gakuya (Embakasi North) na Benjamin Gathiru almaarufu Mejja Donk (Embakasi Central).

“Baada ya kusikiza mawasilisho ya mawakili Danstan Omari na Shadrack Wambui pamoja na kuchambua ushahidi ulioambatishwa na ombi la Gakuya na Gathiri, ni bayana haki zao zitakandamizwa na wako na ombi lililo na mashiko kisheria,” alisema Jaji Mwita.

Jaji Mwita alifahamishwa na mawakili Bw Omari na Bw Wambui, kwamba wanasiasa hao wanalengwa na haki zao kukandamizwa na polisi kwa vile ni wandani wa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

“Hakuna ukweli wowote wawili hawa wanafadhili maandamano ya Gen Z. Kila mtu amepewa idhini ya kuandamana kwa mujibu wa Kifungu nambari 37 cha Katiba kuelezea kutoridhika kwao na uongozi mbaya wa Serikali,” Mabw Omari na Wambui walimweleza Jaji Mwita.

Mawakili hao walimueleza Jaji Mwita kwamba maafisa kutoka kitengo cha DCI na kile cha ujasusi (NIS), waliwatia nguvuni wabunge na kuwanyang’anya simu zao za rununu kwa madai walikuwa wakipanga njama za maandamano na kufadhili uhuni wakati wa maandamano ya Gen Z.

“Inspekta Philip Sang alipata agizo kutoka kwa Hakimu Mkuu wa mahakama ya Kiambu kuchunguza mawasiliano ya simu ya Mabw Gakuya na Gathiru kubaini ukweli wa habari za kijasusi kwamba wawili hao ndio wanaofadhili uhuni wakati wa maandamano ya Gen Z,” Bw Omari alimweleza Jaji Mwita.

Jaji Mwita aliwaagiza mawakili hao wawakabidhi Waziri wa Usalama wa Ndani, IG, DCI na Mwanasheria mkuu nakala za kesi hiyo katika muda wa siku 7 kuanzia Agosti 6, 2024 ndipo wawasilishe majibu mahakamani dhidi ya madai ya kuhujumu haki za Mabw Gakuya na Gathiru.

Tuesday, 6 August 2024

WALZ KUWA TEGEMEO LA HARRIS KATIKA KURA ZA MASHAMBANI ANYOTEGEMEA TRUMP.

 


MGOMBEA urais wa Chama cha Democrat Kamala Harris amemteua Gavana wa Minnesota Tim Walz kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa urais wa Novemba 5, mwaka huu.

Waltz anasifiwa kama mwenye kipawa cha usemi na mtetezi sugu wa sera endelevu nchini Amerika.

Anatarajiwa kumsaidia Harris kuvutia kura katika maeneo ya mashambani na kura za Waamerika weupe.

Hata hivyo, maafisa wa kikosi cha kampeni za makamu huyo wa rais walidinda kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo.

Walz, 60, ambaye ni shujaa wa zamani wa Jeshi la Kitaifa la Amerika na mwalimu, alichaguliwa kama Mbunge katika Bunge la Wawakilishi mnamo 2006 ambako alihudumu kwa miaka 12 kabla ya kuchaguliwa Gavana wa Jimbo la Minnesota mnamo 2018.

Akihudumu kama Gavana, Walz alitetea ajenda endelevu zilizojumuisha utoaji wa lishe shule bila kulipiwa, malengo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, punguzo la ushuru kwa watu wa tabaka la kati na kuanzishwa kwa sera za wafanyakazi kulipwa wakiwa likizoni katika jimbo la Minnesota.

Walz ametetea haki za uzazi za wanawake

Aidha, kwa muda mrefu, Walz ametetea haki za uzazi za wanawake, masilahi ya wadau katika sekta ya kilimo na kuunga mkono haki kuhusu umiliki wa bunduki na raia.

Aliendeleza utetezi huo alipohudumu kama mwakilishi wa eneo la mashambani katika Bunge la Wawakilishi.

Harris, ambaye ni binti ya wahamiaji kutoka Jamaica na India, anatarajia kuwa mwanasiasa kutoka jimbo ambalo wapiga kura wake wengine huunga mkono chama cha Republican katika chaguzi za urais, atamfaa zaidi.

Jimbo hilo la Minnesota pia linapakana na majimbo mawili ya Wisconsin na Michigan, ambayo hushindaniwa kwa ukaribu na chama hicho na kile cha Republican.

Majimbo kama hayo huonekana kama muhimu katika kuamua mshindi katika chaguzi za urais zilizopita sawa na uchaguzi ujao.

Walz anaonekana na wengi kama mwenye ujuzi wa kuwavutia wapiga kura weupe na wale wa maeneo ya mashambani ambao katika miaka michache iliyopita wamemuunga mkono mgombeaji wa chama cha Republican Donald Trump.

Harris alimteua Walz badala ya gavana wa Pennsylvania Josh Shapiro, ambaye alitarajiwa kumpa ushindi katika jimbo hilo muhimu.

Makamu huyo wa Rais aliteuliwa mgombeaji urais wa Chama cha Democrat baada ya bosi wake, Rais Joe Biden kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kutafuta muhula wa pili Ikuluni mwezi jana.

Tangu wakati huo, amechangiwa fedha nyingi za kufadhili na kutoa mwelekeo mpya katika kampeni dhidi ya Trump.

Jumanne jioni, Harris alitarajiwa kujitokeza na mgombea mwenza wake katika mkutano wa kampeni katika mji wa Philadelphia.

Inatarajiwa kuwa tajriba pana ya Walz jeshini na ufanisi wake kama kocha wa kandanda katika shule ya upili itavutia wapiga kura ambao hawataki Trump ahudumu kwa muhula wa pili katika Ikulu ya White House.

Aidha, imeripotiwa kuwa Gavana huyo wa Minnesota alikuwa akiungwa mkono na aliyekuwa Spika wa Bunge Nancy Pelosi, aliyechangia pakubwa katika kumshawishi Rais Biden, 81, ajiondoe kinyang’anyironi.

Harris na Walz sasa watakabana koo na Trump na mgombea mwenza wake JD Vance, ambaye pia ni mwanajeshi wa zamani, katika uchaguzi wa Novemba.

https://technofreak-cooldude.blogspot.com/2009/07/how-to-add-moving-text-to-blog-or.html

 https://technofreak-cooldude.blogspot.com/2009/07/how-to-add-moving-text-to-blog-or.html

GACHAGUA ALIYEMUITA RAILA MAJINA SASA AMMEZEA MATE 2027

 


  1. <div class="scrollbox">

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anasema kuwa yuko tayari kumkumbatia kisiasa Kinara wa Upinzani Raila Odinga na atamfikia ili washirikiane naye katika uchaguzi wa 2027.
  1. </div>

Kauli hiyo ya Bw Gachagua inakuja wakati ambapo Bw Odinga ameanza kushirikiana kisiasa na Rais William Ruto na hata wandani wake wakateuliwa serikalini.

Naibu Rais alisema kuwa mwanasiasa huyo wa upinzani si adui wa Mlima Kenya jinsi ambavyo imekuwa ikifasiriwa huku akidai alipotoshwa ndiposa amekuwa akimpinga katika siasa za nchi.

“Mimi nimekuwa nikibeba ile dhana kwamba Bw Odinga sio mtu wa kuaminiwa au wa kushirikiana naye kisiasa. Ndiyo sababu sisi katika eneo la Mlima tumekuwa tukijitenga naye,” akasema Bw Gachagua.

Alikuwa akizungumza mnamo Jumapili usiku, Agosti 4, 2024 wakati alipokuwa akihojiwa na runinga ya Inooro ambayo inapeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu.

“Kwa sasa nataka ieleweke kwamba Bw Odinga ni mmoja wa marafiki wetu ambao hata tunaweza kushirikiana naye kisiasa siku zijazo. Tumemkumbatia kama jamii kwa sababu Rais Ruto amemleta ndani ya serikali na tutachapa kazi pamoja na hatimaye muda ukifika, tuongee kuhusu ndoa kwa siku zijazo za miereka ya kisiasa,” akaongeza.

Bw Gachagua amekuwa hasimu mkubwa wa kisiasa wa waziri huyo mkuu wa zamani na alikuwa kati ya wanasiasa waliomtahadharisha Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya kufanya kazi na kiongozi huyo wa ODM.

Kile ambacho kimeunganisha Naibu Rais na Bw Odinga kimtazamo ni wote kuunga mkono ugavi wa mapato kwa kutegemea idadi ya watu wala si ukubwa wa eneo.

Wito huo umemweka Bw Gachagua pabaya na baadhi ya wanasiasa katika kambi ya Kenya Kwanza, wengi wakimwona kama anayepigania tu maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya.

“Tumefunguka macho sasa na nitaongoza harakati za kumpendekeza Bw Odinga kama mshirika wetu wa dhati Mlimani kama ilivyokuwa katika kinyang’anyiro cha 2022 akisaidiana na Bw Kenyatta,” akasema.

Wakati wa mahojiano hayo, Naibu Rais alirejelea kauli yake kuwa alikuwa amemwekea Bw Odinga mtego kwenye ikulu.

Alisema ni Rais Ruto ndiye alimshauri ayatoe matamshi hayo na kwa kweli aliwajibika kwa kuwa kiongozi wa nchi na Bw Odinga walikutana Uganda kwa Rais Yoweri Museveni.

Alifunguka na kusema kuwa hatua ya Bw Odinga kuunga kauli yake kuhusu mgao wa rasilimali ni ishara tosha kuwa waziri huyo mkuu wa zamani anafahamu masuala ya uongozi wa nchi hii.

“”Nilikemewa sana hata na viongozi wenzangu wa Mlima Kenya. Lakini nilishangaa kumsikia Bw Odinga akiniunga mkono hadharani,

“Bibi yangu aliniambia kwamba roho imemfunulia kwamba Bw Odinga ni yule malaika wa nia njema ambaye kumtambua ni lazima kuwe na ufunuo. Ufunuo huo ndio hatujawahi kuwa nao kama watu wa Mlima na ndipo tukamchukia,” akasema.

Sifa hizi kochokocho ambazo Bw Gachagua amemiminia Raila zinakuja wakati ambapo kumekuwa na madai kuwa naibu rais anapanga kuanzisha ndoa ya kisiasa na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Licha ya kukita sana siasa zake eneo la Mlima Kenya, wakati wa mahojiano hayo, Bw Gachagua alifunguka na kusema yupo tayari pia kuanzisha ushirikiano na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Kiongozi wa DAP Kenya Eugene Wamalwa.

Kumkumbatia Bw Odinga kuna kuja wakati ambapo washirika wa mbunge huyo wa zamani wa Lang’ata nao wameteuliwa ndani ya serikali kutokana na ukuruba wake na Rais Ruto.

Kando na kutunukiwa mawaziri watano, mwanasheria mkuu mteule Dorcas Oduor pia anatoka Nyanza, ngome ya kisiasa ya Raila.

Pia kuna mabadiliko yanayotarajiwa ya makatibu wanaodumu serikalini ambapo inadaiwa kinara huyo wa upinzani atavuna vinono.

Bw Gachagua mwenyewe amekuwa akilalamika kuwa wandani wake wanahangaishwa na makachero wa Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) pamoja na maafisa kutoka Shirika la Kijasusi (NIS).

Kati ya wandani wake aliosema wamekuwa wakifuatiliwa, kuhangaishwa na mawasiliano yao kurekodiwa ni Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya na mwenzake wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru maarufu kama Meja Donk.

Wakati wa mahojiano hayo, Naibu Rais alionekana kuwa na tofauti kubwa na bosi wake akisema kuwa hata hakuhusishwa au kushauriwa wakati ambapo katibu mkuu wa chama cha UDA, Bw Cleophas Malala aling’atuliwa mamlakani wiki jana.

LUSAKA AMKAUKIA SENETA ONYONKA KWA KUMUITA MPUMBAVU!

 


GAVANA wa Kaunti ya Bungoma, Kenneth Lusaka, Jumatatu, Agosti 5, 2024 alisimamisha kwa muda kikao cha Seneti akitaka Seneta aliyemdhalilisha kwa kumtusi kumuomba msamaha.

Bosi huyo wa gatuzi la Bungoma alifika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi ambapo alitakiwa kujibu maswali kuhusu akaunti za Benki ya Commercial (KCB) zinazoendeshwa na kaunti yake.

Hata hivyo, kabla ya kikao hicho kuanza, Gavana Lusaka alieleza Kamati hiyo kwamba Seneta wa Kisii, Richard Onyonka, alimkosea heshima kwa kumwita ‘mpumbavu” na kumtaka aombe radhi.

Haya yalijiri kufuatia ripoti kuwa usimamizi wa kaunti ya Bungoma ulitumia kitita cha Sh25 milioni kwa urembeshaji, ikiwemo kununua maua wakati wa Sikukuu ya Madaraka, mwaka huu, 2024.

Kulingana na Gavana Lusaka, madai hayo hayana msingi wowote kumruhusu Seneta wa Kisii kumshambulia kwa maneno mazito.

“Mialiko hutokana na ripoti ya mdhibiti wa bajeti, ndiposa tuko hapa. Lakini wakati ambapo suala hata halijashughulikiwa na kamati yoyote, mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, mdhibiti bajeti wala EACC, ni uvumi mitaani. Kisha tunalitumia kuunda taswira fulani si haki kabisa ukijua kuwa nitafika hapa,” alisema Gavana Lusaka.

“Mimi ni binadamu na nilihisi nimedhalilishwa kwa kuitwa mpumbavu. Nataka Seneta aombe radhi kwa matamshi hayo.”

Akijitetea, Seneta Onyonka alifafanua kwamba matamshi yake yalitokana na ghadhabu kuhusu ubadhirifu wa fedha uliokithiri Kaunti ya Bungoma akisema hakulenga nafsi ya Gavana.

“Gavana Lusaka wewe ni mwanamme ninayeheshimu mno, hakuna shaka kuhusu hilo. Nilipoona ripoti kuwa Gavana wa Bungoma alinunua maua ya Sh25 milioni nilipandwa na mori. Haikuwa kukuhusu, kauli hiyo haikukulenga. Ikiwa kauli hiyo ilikukwaza ninaomba radhi kwa dhati,” alisema Seneta Onyonka.

“Lakini nitakwambia leo Gavana, nikija leo katika Kituo cha Afya Bungoma nilipokuwa tukiandamana na mwenyekiti, tulipopata wanawake wamelala sakafuni, nakwambia bado nitasema, ‘hawa ni wapumbavu wanaofanya kazi katika kituo kama hiki.’ Mahali tunapowachukulia watu wetu maskini kwa kiwango duni zaidi kuliko tunavyowatendea mbwa wetu.”

Alisema matamshi yake hayakumlenga Gavana Lusaka bali “mifumo mibovu ya taifa langu, Kenya ambapo unasimamia karibu bilioni moja za kufadhili huduma za matibabu na wanawake wote katika kituo hicho…”

“Ukija hapa, huji ili tukueleze jinsi tulivyo safi nawe una hatia. Ni mdahalo jinsi ulivyosema. Uhalisia ni kuwa tulikuwa Bungoma na watu walikuwa wamelala sakafuni tulipoingia. Ukweli ni ule ule ila matamshi, tukizingatia hadhi yako, ninataka kusema samahani kwamba nilikusawiri hivyo.”

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Wajir, Abass Mohamed, ilielezwa kuwa, Gavana Lusaka vilevile amenukuliwa akitoa matamshi ya kudhalilisha viongozi wengine wakiwemo maseneta.

“Natoka kaunti anayotoka Gavana. Juzi alisema ukiona kobe juu ya meza bila shaka kuna mtu aliyeiwekelea hapo. Lakini sitaichukulia binafsi kwa sababu hatimaye kobe yuko hapa. Tusichukulie mambo kwa kibinafsi,” alisema Seneta Onyonka.

Monday, 5 August 2024

GEN Z WA BANGALADESH WAVAMIA IKULU YA WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina Wazed amejiuzulu na kuondoka nchini humo, baada ya wiki kadhaa za maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi na kupelekea machafuko makubwa nchini kote. Ripoti zinasema, bibi huyo mwenye umri wa miaka 76 alikimbia kwa helikopta Jumatatu hadi India, wakati maelfu ya waandamanaji wakivamia makazi yake katika mji mkuu wa Dhaka. Hilo limemaliza utawala wa Waziri Mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi nchini Bangladesh, kwa zaidi ya miaka 20 jumla. Anasifiwa kwa kusimamia maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo ya Kusini mwa Asia, hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni Bi Hasina ameshutumiwa kwa kugeuka kuwa kiongozi wa kiimla. Aliingiaje madarakani? Alizaliwa katika familia ya Kiislamu huko Bengal Mashariki mwaka 1947, Bi Hasina anatokea familia ya wanasiasa. Baba yake Sheikh Mujibur Rahman, 'Baba wa Taifa' la Bangladesh, alikuwa kiongozi mzalendo aliyeongoza uhuru wa nchi hiyo kutoka Pakistan mwaka 1971 na kuwa rais wa kwanza. Wakati huo, Bi Hasina alikuwa tayari anajuulikana kwa kuwa kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dhaka. Rahman aliuawa pamoja na watu wengi wa familia yake katika mapinduzi ya kijeshi mwaka 1975. Bi Hasina na dadake mdogo ndio pekee walionusurika kwani walikuwa safarini nje ya nchi wakati huo. Baada ya kuishi uhamishoni nchini India, Bi Hasina alirejea Bangladesh mwaka 1981 na kuwa kiongozi wa chama cha kisiasa cha babake, Awami League. Aliungana na vyama vingine vya kisiasa kufanya maandamano mitaani ya kuunga mkono demokrasia, wakati wa utawala wa kijeshi wa Jenerali Hussain Muhammed Ershad. Vuguvugu hilo lilimfanya Bi Hasina akawa mwanasiasa wa kitaifa haraka sana. Aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1996. Alipata sifa kwa kutia saini mkataba wa kugawana maji na India na mapatano ya amani na waasi kusini-mashariki mwa nchi hiyo. Lakini wakati huo huo, serikali yake ilikosolewa kwa mikataba mingi ya kibiashara inayodaiwa kuwa ni mbovu na kwa kuwa mtiifu sana kwa India. Baadaye alishindwa na mshirika wake wa zamani aliyegeuka kuwa mpinzani, Bi Begum Khaleda Zia wa chama cha Bangladesh Nationalist Party (BNP), mwaka 2001. Wanawake wote wawili wametawala siasa za Bangladesh kwa zaidi ya miongo mitatu na wanajulikana kama "Begums wanaovutana." Begum ina maana ya mwanamke wa Kiislamu wa daraja la juu. Waangalizi wanasema ushindani wao mkali umesababisha mlipuko wa mabomu katika mabasi, kutoweka na mauaji ya kiholela ya mara kwa mara. Bi Hasina hatimaye alirejea mamlakani mwaka 2009 katika uchaguzi uliofanyika chini ya serikali ya mpito. Akiwa mwathirika wa kisiasa, amekamatwa mara kadhaa akiwa upinzani na vile vile majaribio kadhaa ya kumuua, likiwemo moja la mwaka 2004 ambalo liliharibu usikivu wake. Pia amenusurika juhudi za kumlazimisha Kwenda uhamishoni kwa kesi nyingi mahakamani zinazomshutumu kwa ufisadi. Mafanikio yake ni yapi? Bangladesh, taifa lenye Waislamu wengi, lilikuwa mojawapo ya mataifa maskini zaidi duniani, limepata mafanikio makubwa ya kiuchumi chini ya uongozi wake tangu 2009. Sasa ni moja wapo ya taifa lenye uchumi unaokua kwa kasi katika eneo hilo, hata kupita jirani yake mkubwa India. Pato la taifa kwa mtu mmoja limeongezeka mara tatu katika muongo uliopita na Benki ya Dunia inakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 25 wameondokana na umaskini katika miaka 20 iliyopita. Sehemu kubwa ya ukuaji huu imechochewa na sekta ya nguo, ambayo inachangia idadi kubwa ya mauzo ya nje ya nchi na sekta hiyo imekuwa katika miongo ya hivi karibuni, ikisambaza nguo katika masoko ya Ulaya, Amerika Kaskazini na Asia. Serikali ya Bi Hasina imefanya miradi mikubwa ya miundombinu kwa kutumia fedha za nchi hiyo, mikopo na usaidizi wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na daraja kubwa la Padma lililogharimu dola za kimarekani bilioni 2.9 huko Ganges.

AJALI SACHANGWAN HUKU WANAFUNZI 25 NA WAALIMU 3 WAKIPATA MAJERAHA MABAYA

WANAFUNZI 26, walimu watatu na mpishi mmoja wa shule ya Rockside Academy, Nairobi wanapokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru na Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Molo baada ya gari lao kuhusika katika ajali eneo la Sachangwan, Nakuru, Jumatatu, Agosti 5, 2024. Kwa mujibu wa Kamanda ya Polisi wa Kaunti Ndogo ya Molo Timon Odingo, basi hilo la shule lilikuwa likiwasafirisha wanafunzi kutoka Eldoret ambako walikuwa wameshiriki tamasha za muziki zinazoendelea. Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa saba za mchana baada ya lori kutoka nyuma kupoteza mwelekeo na kugonga basi hilo kutoka nyuma. Baadaye lori hilo liligonga magari mengine mawili ya kibinafsi hadi yakaanguka kwenye mtaro kando ya barabara. Watu 30 walipata majeraha katika ajali hiyo, japo waliokuwa kwenye magari ya kibinafsi hawakuathiriwa. Maafisa wa polisi walipowasili katika eneo la ajali wenyeji na wasamaria wema walikuwa tayari wamewaondoa waathiriwa. “Waliojeruhiwa wamekimbizwa hospitalini na sasa wanapokea matibabu. Kwa bahati nzuri hakuna aliyekufa. Maafisa wa polisi wametumwa hospitali kuendeleza uchunguzi,” Bw Odingo akasema.

Friday, 19 July 2024

RAIS RUTO AKOSOLEWA KWENYE BARAZA LAKE JIPYA LA WATU 11 AKIWAHUSISHA WALIOFURUSHWA

Rais william ruto hatimaye ametangaza baraza la mawazi ambayo kwa sasa inakosolewa pakubwa na watu mbalimbali.je atayaweza Interior - Kithure Kindiki Health - Dr. Debra Mulongo Barasa Public Works - Alice Wahome Education - Julius Ogamba Defence - Aden Duale Agriculture - Dr. Andrew Karanja Environment - Soipan Tuya Water - Eric Muriithi Roads - Davis Chirchir ICT - Dr. Margaret Ndungu AG - Rebecca Miano

Wednesday, 17 July 2024

KITUO CHA PEPEA RADIO SASA YASIKIKA VYEMA MTANDAONI

Sasa unawezasikiliza pepea radio inakuwa kivutio kikubwa kwenye mtandao kwa burudani tosha.bonyeza tu hii link hapa upate uhondo https://zeno.fm/radio/pepea-radio/ ama tafuta tu PEPEA RADIO kwenye google search

WANAHABARI WAPANGA MAANDAMANO TAREHE 24 JULAI

JUMATANO, Julai 24, 2024, itakuwa zamu ya wanahabari kujitokeza barabarani kote nchini kwa maandamano ya kupinga dhuluma wanazotendewa na polisi wakiwa kazini. Akitoa ilani kuhusu maandamano hayo, rais wa Chama cha Wahariri Nchini (KEG) Zubeida Kananu Jumatano alilaani visa vya wanahabari kushambuliwa na polisi wakiwa kazini akisema vinahujumu uhuru wao ambao unalindwa na katiba. Bi Kananu alitoa mifano ya visa vya hivi punde vya kupigwa risasi kwa ripota wa Shirika la Habari la Mediamax Catherine Wanjeri Kariuki na polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Nakuru na kutekwa nyara kwa mwanahabari mkongwe Macharia Gaitho na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa polisi. “Kwa hivyo, tumekubaliana kwamba mnamo Jumatano wiki ijayo wanahabari watafanya maandamano kulaani vitendo kama hivi vya kikatili wanavyotendewa na polisi wanapotekeleza majukumu yao,” akasema alipoandamana na Bw Gaitho kuandikisha taarifa katika Afisi za Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA). Hii ni kufuatia kisa cha Jumatano asubuhi ambapo mwanahabari huyo alitekwa mara na watu waliodai kuwa wao ni maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI). Bw Gaitho alitendewa unyama huo katika Kituo cha Polisi cha Karen alikokimbilia baada ya kubaini kuwa alikuwa akiandamwa na maafisa hao waliokuwa kwenye gari la kibinafsi. Hata hivyo, baadaye DCI ilitoa taarifa ikidai maafisa wake walimkamata Bw Gaitho kimakosa kwani walikuwa wakimlenga mwanablogu Francis Gaitho. Bi Kananu alisema kuwa maandamano ya wanahabari yatakuwa ya amani na washiriki hawajihami kwa vitu vya kutishia amani. “Hatutajihami kwa mawe wala marungu, bali tutabeba kamera zetu, vijitabu na kalamu miongoni mwa vyombo vingine vya kazi. Sharti ulimwengu mzima ujue maovu yanayotendewa wanahabari nchini Kenya,” Bi Kananu akasema, akisisitiza. Katibu Mkuu wa Muungano wa Wanahabari Nchini (KUJ) Eric Oduor amethibitisha mipango ya maandamano hayo na kuwataka wanahabari wote nchini kushiriki. “Tutamjulisha rasmi Kaimu Inspekta Jenerali Douglas Kanja kuhusu nia yetu ya wanachama wetu kufanya maandamano kote nchini Jumatano wiki ijayo kupinga mwenendo wa polisi kushambulia wanachama wetu wakiwa kazini,” Bw Odour akaambia umma kwa njia ya simu.

SIMANZI KENYA JAJI OGEMBO AAGA DUNIA

Marehemu Jaji Daniel Ogembo, alipatikana Jumatano, Julai 17, 2024 akiwa ameaga dunia katika makazi yake rasmi mjini Siaya. Alitarajiwa kuongoza kikao asubuhi katika majengo ya Mahakama Kuu ya Siaya lakini akakosa kujitokeza hali iliyoibua shaka. Jaji Ogembo amehudumu kwa miaka miwili katika Mahakama Kuu ya Siaya alipokuwa jaji mkazi. Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Siaya, Cleti Kimaiyo, alithibitisha kifo chake na kusema polisi na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo. “Tutawafahamisha kuhusu matokeo, bado tunachunguza kiini cha kifo chake,” alisema mkuu wa polisi kaunti hiyo. Kulingana na afisa mmoja wa mahakama aliyechelea kutajwa kwa sababu ya uzito wa suala hilo, Jaji Ogembo alipatikana akiwa mfu asubuhi baada ya kukosa kujibu dereva wake alipokwenda kumchukua nyumbani kwake. “Dereva alimpeleka nyumbani Jumanne jioni lakini aliporejea asubuhi, jaji hakujibu hali iliyofanya dereva kuripoti kwa maafisa katika korti ya Siaya,” alisema afisa huyo wa ngazi ya juu. Kifo cha Jaji Ogembo kililemaza vikao vya korti huku wafanyakazi wakikumbwa na mshtuko kufuatia habari hizo. Kifo cha Jaji Ogembo kimetokea hata kabla ya wiki kuisha baada ya Jaji David Majanja kufariki dunia. Mwezi uliopita, Hakimu Mkuu wa Korti ya Makadara, Monicah Kivuti, aliuawa kwa kupigwa risasi na afisa mkuu wa polisi kutoka kituo cha Londiani.

Friday, 30 June 2023

PEPEA RADIO NOW ONLINE

first started like ajoke but finally the dream has become true.A radio owned by TRANSMEDIA AFRICA LTD. Is set to be launched offgicially soon as it has already started airing its programmes.Peter Mukabi the owner of the statio reteriated that he consider mostly creativ mind.He told our newsdesk the radio stion wilat large cover news,east africa music and other related things.Peter Mukabi is one of the longest serving radio journalist in kenya. Sources indicates that most people across the world now tune into the stion.Mukabi revealed to us that he will be streaming alsso church events so that to reach deaper audiency.Talented youths are also encouraged to send application and proposalPeter Mukabi is the CEO of the statio