Wednesday, 17 July 2024
WANAHABARI WAPANGA MAANDAMANO TAREHE 24 JULAI
JUMATANO, Julai 24, 2024, itakuwa zamu ya wanahabari kujitokeza barabarani kote nchini kwa maandamano ya kupinga dhuluma wanazotendewa na polisi wakiwa kazini.
Akitoa ilani kuhusu maandamano hayo, rais wa Chama cha Wahariri Nchini (KEG) Zubeida Kananu Jumatano alilaani visa vya wanahabari kushambuliwa na polisi wakiwa kazini akisema vinahujumu uhuru wao ambao unalindwa na katiba.
Bi Kananu alitoa mifano ya visa vya hivi punde vya kupigwa risasi kwa ripota wa Shirika la Habari la Mediamax Catherine Wanjeri Kariuki na polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Nakuru na kutekwa nyara kwa mwanahabari mkongwe Macharia Gaitho na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa polisi.
“Kwa hivyo, tumekubaliana kwamba mnamo Jumatano wiki ijayo wanahabari watafanya maandamano kulaani vitendo kama hivi vya kikatili wanavyotendewa na polisi wanapotekeleza majukumu yao,” akasema alipoandamana na Bw Gaitho kuandikisha taarifa katika Afisi za Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA).
Hii ni kufuatia kisa cha Jumatano asubuhi ambapo mwanahabari huyo alitekwa mara na watu waliodai kuwa wao ni maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Bw Gaitho alitendewa unyama huo katika Kituo cha Polisi cha Karen alikokimbilia baada ya kubaini kuwa alikuwa akiandamwa na maafisa hao waliokuwa kwenye gari la kibinafsi.
Hata hivyo, baadaye DCI ilitoa taarifa ikidai maafisa wake walimkamata Bw Gaitho kimakosa kwani walikuwa wakimlenga mwanablogu Francis Gaitho.
Bi Kananu alisema kuwa maandamano ya wanahabari yatakuwa ya amani na washiriki hawajihami kwa vitu vya kutishia amani.
“Hatutajihami kwa mawe wala marungu, bali tutabeba kamera zetu, vijitabu na kalamu miongoni mwa vyombo vingine vya kazi. Sharti ulimwengu mzima ujue maovu yanayotendewa wanahabari nchini Kenya,” Bi Kananu akasema, akisisitiza.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Wanahabari Nchini (KUJ) Eric Oduor amethibitisha mipango ya maandamano hayo na kuwataka wanahabari wote nchini kushiriki.
“Tutamjulisha rasmi Kaimu Inspekta Jenerali Douglas Kanja kuhusu nia yetu ya wanachama wetu kufanya maandamano kote nchini Jumatano wiki ijayo kupinga mwenendo wa polisi kushambulia wanachama wetu wakiwa kazini,” Bw Odour akaambia umma kwa njia ya simu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment