Naibu Rais Gachagua kwenye picha |
MAHAKAMA Kuu imeamuru polisi wasiwatie nguvuni wabunge wawili wanaodaiwa kufadhili maandamano ya vijana yaliyopelekea watu zaidi ya 60 kuuawa na zaidi ya watu 600 kujeruhiwa.
Jaji Enock Chacha Mwita aliwaamuru Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin wasiwakamate Wabunge James Mwangi Gakuya (Embakasi North) na Benjamin Gathiru almaarufu Mejja Donk (Embakasi Central).
“Baada ya kusikiza mawasilisho ya mawakili Danstan Omari na Shadrack Wambui pamoja na kuchambua ushahidi ulioambatishwa na ombi la Gakuya na Gathiri, ni bayana haki zao zitakandamizwa na wako na ombi lililo na mashiko kisheria,” alisema Jaji Mwita.
Jaji Mwita alifahamishwa na mawakili Bw Omari na Bw Wambui, kwamba wanasiasa hao wanalengwa na haki zao kukandamizwa na polisi kwa vile ni wandani wa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
“Hakuna ukweli wowote wawili hawa wanafadhili maandamano ya Gen Z. Kila mtu amepewa idhini ya kuandamana kwa mujibu wa Kifungu nambari 37 cha Katiba kuelezea kutoridhika kwao na uongozi mbaya wa Serikali,” Mabw Omari na Wambui walimweleza Jaji Mwita.
Mawakili hao walimueleza Jaji Mwita kwamba maafisa kutoka kitengo cha DCI na kile cha ujasusi (NIS), waliwatia nguvuni wabunge na kuwanyang’anya simu zao za rununu kwa madai walikuwa wakipanga njama za maandamano na kufadhili uhuni wakati wa maandamano ya Gen Z.
“Inspekta Philip Sang alipata agizo kutoka kwa Hakimu Mkuu wa mahakama ya Kiambu kuchunguza mawasiliano ya simu ya Mabw Gakuya na Gathiru kubaini ukweli wa habari za kijasusi kwamba wawili hao ndio wanaofadhili uhuni wakati wa maandamano ya Gen Z,” Bw Omari alimweleza Jaji Mwita.
Jaji Mwita aliwaagiza mawakili hao wawakabidhi Waziri wa Usalama wa Ndani, IG, DCI na Mwanasheria mkuu nakala za kesi hiyo katika muda wa siku 7 kuanzia Agosti 6, 2024 ndipo wawasilishe majibu mahakamani dhidi ya madai ya kuhujumu haki za Mabw Gakuya na Gathiru.
No comments:
Post a Comment