HABARI KUU:

GACHAGUA ALIYEMUITA RAILA MAJINA SASA AMMEZEA MATE 2027..//..LUSAKA AMKAUKIA SENETA ONYONKA KWA KUMUITA MPUMBAVU!..//..GEN Z WA BANGALADESH WAVAMIA IKULU YA WAZIRI MKUU..//..AJALI SACHANGWAN HUKU WANAFUNZI 25 NA WAALIMU 3 WAKIPATA MAJERAHA MABAYA..//..MGOMBEA urais wa Chama cha Democrat Kamala Harris amemteua Gavana wa Minnesota Tim Walz kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa urais wa Novemba 5, mwaka huu.// AMERIKA imeonya serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi kukabili waandamanaji na kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu..//GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza anataka Mahakama Kuu kuwahukumu maafisa wawili wa bunge la kaunti na MCA aliyeteuliwa kwa madai walidharau mahakama, akisema walipuuza maagizo ya korti kwa kukusudia kumtimua kwa mara ya tano.

Tuesday, 6 August 2024

WALZ KUWA TEGEMEO LA HARRIS KATIKA KURA ZA MASHAMBANI ANYOTEGEMEA TRUMP.

 


MGOMBEA urais wa Chama cha Democrat Kamala Harris amemteua Gavana wa Minnesota Tim Walz kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa urais wa Novemba 5, mwaka huu.

Waltz anasifiwa kama mwenye kipawa cha usemi na mtetezi sugu wa sera endelevu nchini Amerika.

Anatarajiwa kumsaidia Harris kuvutia kura katika maeneo ya mashambani na kura za Waamerika weupe.

Hata hivyo, maafisa wa kikosi cha kampeni za makamu huyo wa rais walidinda kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo.

Walz, 60, ambaye ni shujaa wa zamani wa Jeshi la Kitaifa la Amerika na mwalimu, alichaguliwa kama Mbunge katika Bunge la Wawakilishi mnamo 2006 ambako alihudumu kwa miaka 12 kabla ya kuchaguliwa Gavana wa Jimbo la Minnesota mnamo 2018.

Akihudumu kama Gavana, Walz alitetea ajenda endelevu zilizojumuisha utoaji wa lishe shule bila kulipiwa, malengo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, punguzo la ushuru kwa watu wa tabaka la kati na kuanzishwa kwa sera za wafanyakazi kulipwa wakiwa likizoni katika jimbo la Minnesota.

Walz ametetea haki za uzazi za wanawake

Aidha, kwa muda mrefu, Walz ametetea haki za uzazi za wanawake, masilahi ya wadau katika sekta ya kilimo na kuunga mkono haki kuhusu umiliki wa bunduki na raia.

Aliendeleza utetezi huo alipohudumu kama mwakilishi wa eneo la mashambani katika Bunge la Wawakilishi.

Harris, ambaye ni binti ya wahamiaji kutoka Jamaica na India, anatarajia kuwa mwanasiasa kutoka jimbo ambalo wapiga kura wake wengine huunga mkono chama cha Republican katika chaguzi za urais, atamfaa zaidi.

Jimbo hilo la Minnesota pia linapakana na majimbo mawili ya Wisconsin na Michigan, ambayo hushindaniwa kwa ukaribu na chama hicho na kile cha Republican.

Majimbo kama hayo huonekana kama muhimu katika kuamua mshindi katika chaguzi za urais zilizopita sawa na uchaguzi ujao.

Walz anaonekana na wengi kama mwenye ujuzi wa kuwavutia wapiga kura weupe na wale wa maeneo ya mashambani ambao katika miaka michache iliyopita wamemuunga mkono mgombeaji wa chama cha Republican Donald Trump.

Harris alimteua Walz badala ya gavana wa Pennsylvania Josh Shapiro, ambaye alitarajiwa kumpa ushindi katika jimbo hilo muhimu.

Makamu huyo wa Rais aliteuliwa mgombeaji urais wa Chama cha Democrat baada ya bosi wake, Rais Joe Biden kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kutafuta muhula wa pili Ikuluni mwezi jana.

Tangu wakati huo, amechangiwa fedha nyingi za kufadhili na kutoa mwelekeo mpya katika kampeni dhidi ya Trump.

Jumanne jioni, Harris alitarajiwa kujitokeza na mgombea mwenza wake katika mkutano wa kampeni katika mji wa Philadelphia.

Inatarajiwa kuwa tajriba pana ya Walz jeshini na ufanisi wake kama kocha wa kandanda katika shule ya upili itavutia wapiga kura ambao hawataki Trump ahudumu kwa muhula wa pili katika Ikulu ya White House.

Aidha, imeripotiwa kuwa Gavana huyo wa Minnesota alikuwa akiungwa mkono na aliyekuwa Spika wa Bunge Nancy Pelosi, aliyechangia pakubwa katika kumshawishi Rais Biden, 81, ajiondoe kinyang’anyironi.

Harris na Walz sasa watakabana koo na Trump na mgombea mwenza wake JD Vance, ambaye pia ni mwanajeshi wa zamani, katika uchaguzi wa Novemba.

No comments:

Post a Comment