MAHAKAMA ya Mazingira na Ardhi imetoa uamuzi ambapo mwanamke mmoja anatakiwa kulipa kanisa la Katoliki Dayosisi ya Nakuru Sh23 Milioni.
Sasa mwanamke huyo anatakiwa kurejesha pesa alizopokea kwa njia ya ulaghai baada ya kushtakiwa kwa kuuzia kanisa ardhi hewa.
Jaji Anthony Ombwayo alimwagiza Bi Hannah Wairimu Kahiga alipe pesa hizo zinazojumuisha Sh 19,800,000 ambazo kanisa lililipa kwa ununuzi wa shamba la ekari 11 katika eneo la Kiambogo, kaunti ndogo ya Naivasha na Sh 3, 960,000 kama fidia.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya kubainika kuwa mshtakiwa aliuza shamba la mtu mwingine kwa kutumia hati bandia.
Bi Hannah Wairimu anadaiwa kushirikiana na maafisa katika afisi ya ardhi kuuza shamba hilo la ekari 11 ambalo ni sehemu ya shamba la Teresia Wanjiru Wangera aliyefariki 1981.
“Mshtakiwa wa Kwanza (Bi Wairimu) hajathibitisha kwa mahakama hii kwamba alipata hatimiliki kihalali na kiutaratibu alipouza mali hiyo kwa Mlalamishi (Kanisa Katoliki),” Jaji Ombwayo akaamua.
Kanisa kupitia wadhamini wake waliosajiliwa ambao maafisa wao wa sasa ni Maurice Muhatia, Askofu Mkuu Kisumu, baba Lawrence Mbogo na baba Simon Kamau walimwendea Bi Wairimu kwa nia ya kununua ardhi hiyo kwa mradi wa kanisa.
No comments:
Post a Comment