MGOMBEAJI wa urais wa chama cha Republican, Donald Trump, Jumatano alishambulia sera za mpinzani wake wa chama cha Democratic, Kamala Harris, katika hotuba aliyotoa akiwa Asheville, North Carolina huku kura za maoni zikionyesha umaarufu wake unazidi kupungua.
Baadhi ya washirika, wafadhili, na washauri walionyesha wasiwasi kuhusu mashambulizi ya Trump kwa makamu huyo wa rais wa Amerika na kupendekeza alenge sera zilizofeli ambazo Harris alitetea akiwa afisini.
Akihutubia wafuasi wake, Trump aliepuka mashambulizi kuhusu rangi ya Harris na kuzamia sera zaidi kinyume na awali.
Lakini aliendelea kumtupia matusi ya kibinafsi, kwa kumuita mshenzi na kukejeli kicheko chake, akisema mpinzani wake ana shida kubwa.
Kujiondoa kwa Rais Joe Biden kwenye kinyang’anyiro cha urais Novemba 5 na kumuidhinisha Harris, mwezi uliopita, kulileta wimbi jipya katika kampeni.
Kura za maoni zinaonyesha Harris anaziba pengo la umaarufu dhidi ya Trump. Baadhi ya kura hizo zinaonyesha Harris yuko mbele katika kinyang’anyiro hicho cha Novemba 5.
Ujio wa Harris ulivuruga kampeni ya Trump, ambaye awali alitumia matusi huku akimlenga Makamu wa Rais ambaye mama yake alizaliwa India na baba yake Jamaica.
Trump alisema kuwa ataidhinisha hivyo basi kurahisisha mchakato wa kutoa vibali vya uchimbaji mafuta pamoja na kupunguza bei iwapo atamshinda Harris.
Pia aliahidi kupunguza bei za nishati na umeme kwa nusu, ndani ya miezi 12 hadi 18, baada ya kuingila mamlakani.
Hakubainisha wazi jinsi atakavyofanya hivyo, lakini alirudia ahadi za awali za kuongeza uzalishaji wa mafuta, ikiwemo katika Hifadhi ya Kitaifa ya Wanyamapori ya Artic, Alaska, ambapo utawala wa Biden ulisitisha utoaji wa vibali vipya.
Alimshutumu Harris kwa kuunga mkono marufuku ya kuchimba mafuta kwa kutumia teknolojia mwaka wa 2019 akisema msimamo wake utakuwa tatizo kubwa katika jimbo muhimu la Pennsylvania.
Kabla ya mkutano wa Trump huko Asheville, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampeni ya Harris, Michael Tyler, alituma taarifa akimshutumu Trump kwa kupuuza tabaka la kati kwa kupinga ulinzi wa vyama vya wafanyakazi na kuunga mkono kupunguzwa kwa ushuru wa makampuni.
Tyler alisema Harris atafanya ziara yake North Carolina, atakapozungumzia sera za kiuchumi katika hotuba yake huko Raleigh.
“Ataeleza mpango wa kupunguza gharama kwa familia za tabaka la kati na atakavyoshughulikia ushuru wa makampuni,” alisema Tyler.