MAAFISA wa upelelezi wanakusanya maelezo yanayotarajiwa kusaidia kutegua kitendawili kuhusu chanzo cha moto kilichosababisha vifo vya wanafunzi 21 katika Shule ya Hillside Endarasha Academy, Kieni, Nyeri.
Miili ilipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Naromoru Level Four kufanyiwa ukaguzi na vipimo vya chembechembe za DNA kuitambua.
Mwanapatholojia wa serikali Dkt Johansen Oduor, Jumapili alisema vipimo vya DNA vitaanza kufanywa, Jumatatu, Septemba 9, 2024.
Jumapili, wahudumu katika hifadhi hiyo ya maiti walikuwa wakiandaa miili hiyo kabla ya wanapatholojia kuwasili.
Hifadhi hiyo inaendelea kujengwa na haijakamilika.
Maswali
Maswali yameulizwa kuhusu chanzo cha moto huo japo madai yameibuliwa kuwa huenda ulisababishwa na kulipuka kwa balbu ya stima.
Hata hivyo kuna wazazi ambao wamepinga nadharia hiyo, wakidai Alhamisi wanafunzi walidaiwa kuibua malalamishi kuhusu masuala fulani shuleni humo.
Mzazi aliyeongea na Taifa Leo Dijitali, na akaomba tulibane jina lake, alisema alipata habari hizo kutoka kwa mwanawe ambaye ni mwanafunzi wa kutwa.
Alisema mvulana huyo wa Gredi 7, alimweleza kuwa mwendo wa saa kumi za jioni baadhi ya wanafunzi walikaa “kwa muda mrefu” katika bweni lililoteketea “wakijadili masuala fulani” ambayo sio ya kawaida.
Usimamizi wa shule hiyo haujatoa taarifa zozote tangu kutokea kwa mkasa huo.
“Baadhi ya wanafunzi walikaa kwa muda mrefu katika bweni na mwanangu aliniambia kulikuwa na wasiwasi shuleni kuhusu mambo yasiyojulikana.
Watoto huwa hawaruhusiwi kwenda katika bweni nyakati za mchana. Wakitaka kwenda huko, sharti waandamane na msimamizi wa mabweni wachukue kile wanachotaka kisha warejee madarasani mara moja. Mbona kanuni hii haikuzingatiwa?”, akauliza.Mzazi huyo pia alisema kuwa mwendo wa saa nne usiku, kuna mwanafunzi aliyempigia simu mzazi wake na kupasha habari kuhusu kutokea kwa moto.
“Swali ni je, simu hiyo ilikuwa ya nani na ni mzazi yupi huyu alipigiwa simu?” mzazi huo akauliza.
“Tunafahamu fika kwamba watoto hawaruhusiwi kutumia simu za mkono wakiwa shule na hufanya hivyo tu baada ya kupata kibali maalum na chini ya usimamizi wa mwalimu mhusika. Tunataka mzazi huyu aliyepigiwa simu ajitokeze na kutoa maelezi kwa maafisa wa upelelezi ili ibainike kilichotendeka.” Mzazi huyo akasema.
Maafisa hao wa upelelezi wa vifo, wakiongozwa na Martin Nyuguto, waliendelea kusaka ushahidi katika eneo la mkasa huku serikali ikisema watoto 48 bado hawajulikani waliko kufikia Jumapili, Septemba 8, 2024 jioni.
Lakini Ijumaa Septemba 6, 2024, Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema watoto 70 hawakujulikana waliko.
Alibashiri kuwa walipewa hifadhi katika makazi ya karibu na Shule ya Hillside Endarasha Academy, walikokimbilia moto ulipotokea.
Jumapili, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nyeri, Anthony Muheria, alitoa wito kwa wazazi waliwachukua watoto baada ya mkasa kupiga ripoti kwa maafisa wa usalama ili kuzima dukuduku kuhusu idadi ya watu ambao hawajulikani waliko.
“Ikiwa mtoto wako yuko nyumbani wapashe maafisa wa upelelezi ili wajue kwamba wako salama. Watoto hao pia wanafaa kupewa ushauri nasaha kutokana na mshtuko uliowapata wakati wa mkasa huo wa moto,” Askofu Muheria akasema wakati wa ibada ya pamoja na kuombea waliofuka na kuzifariji jamaa zilizopoteza watoto wao.
No comments:
Post a Comment