MKUU wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi anaelekea Namibia ambako anatarajiwa kumpigia debe Raila Odinga katika azma yake ya kutaka achaguliwe mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Bw Mudavadi, ambaye aliondoka Jumapili pia ameratibiwa kufanya mashauriano na viongozi wakuu wa Namibia akilenga kuimarisha mahusiano kati ya Kenya na nchi hiyo katika nyanja kadhaa za kimaendeleo.
Hata hivyo, afisi yake ilisema kwenye taarifa kwamba ajenda kuu ya ziara yake ni kumpigia debe Bw Odinga atakapokutana Makamu wa Rais wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah.
“Mudavadi atatumia nafasi hiyo kuvumisha azma ya Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) mnamo Februari 2025,” ikasema taarifa iliyotumwa kwa vyombo na Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari katika afisi ya Mudavadi Jacob Ng’etich.
Ziara hii ni ya kwamba ya kusaka uungwaji mkono kwa Bw Odinga katika eneo la Afrika Kusini baada ya kuzinduliwa kwake jijini Nairobi.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi ilihudhuriwa na baadhi ya marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kenya imewasilisha mwaniaji wa uenyekiti wa AUC kwa mara ya pili mfufulizo baada ya aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni Amina Mohamed kushindwa na mwenyekiti anayeondoa Moussa Faki Mahamat mnamo 2017.
Bw Odinga anashindana na wagombeaji wengine watatu ambao ni Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mohamoud Ali Youssouf, aliyekuwa waziri wa masuala ya kigeni wa Mauritius Anil Kumarsigh Gayan na Waziri wa zamani wa Masuala ya Kigeni wa Madagascar Richard Randriamandrato.
Hata hivyo, inabashiriwa kuwa Youssouf ambaye amehudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni kwa miaka 10 ndiye mshindani mkuu wa Bw Odinga.
Ziara ya Mudavadi nchini Namibia inajiri baada ya Bw Odinga kuungana na ujumbe wa Rais William Ruto katika mkutano wa mashauriano kati ya marais wa Afrika na China kuhusu masuala ya maendeleo (FOCAC) wiki jana jijini Beijing, China.
Wakati wa mkutano huo, Rais Ruto alifanya mikutano tofauti na marais sita wa Afrika kumpigia debe Bw Odinga.
Kando na kumfanyia kampeni Bw Odinga, Bw Mudavadi anatarajiwa kutetea kuimarishwa kwa mahusiano kati ya Kenya na Namibia na kuanzisha kwa ubalozi wa Kenya jijini Nairobi.
Aidha, atatetea kuimarishwa kwa biashara kati ya Kenya na Namibia kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Kulingana na ripoti kutoka kwa Wizara za Masuala ya Kigeni na Biashara nchini Kenya imekuwa ikiagiza bidhaa za thamani ya Sh117.76 milioni kutoka Namibia na kuuza bidhaa za thamani ya Sh106.31 milioni nchini Namibia ndani ya kipindi cha mwongo mmoja.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga
No comments:
Post a Comment