Sunday, 15 September 2024
MOTO WATEKETEZA SHULE MACHAKOS JUMAPILI
MKASA wa moto umeripotiwa katika Shule ya Upili ya Katoloni iliyoko Kaunti ya Machakos.
Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini (KRC), moto huo ulitokea dakika chache baada ya saa tatu za usiku wa Jumamosi, Septemba 14, 2024.
“Kisa cha moto kimeripotiwa katika Shule ya Upili ya Katoloni iliyoko Kaunti ya Machakos. Juhudi za kuuzima zinaendelea,” KRC ikasema kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya X.
Hata hivyo, baadaye wafanyakazi wa shirika hilo la kushughulikia majanga wakishirikiana na wale wa Idara ya Zimamoto katika serikali ya Kaunti ya Machakos walifaulu kudhibiti na kuzima moto huo.
“Shirika la Msalaba Mwekundu pia linatoa huduma ya kwanza katika eneo la tukio,” KRC iliandika kwenye X, baada ya muda wa saa tatu.
Duru zinasema kuwa wanafunzi wawili walikimbizwa katika Hospitali ya Machakos Level 5, baada ya kuathiriwa na moshi uliotokana na moto huo.
Visa kadhaa vya moto kuteketeza mali vimeripotiwa katika shule kadha nchini mwezi huu wa Septemba.
Mkasa mbaya zaidi ulikuwa ni ule uliotokea usiku wa kuamkia Ijumaa, Septemba 6, 2024 Hillside Endarasha Academy, Nyeri ambapo jumla ya wanafunzi 17 walikufa papo hapo.
Wengine wanne walikufa hospitalini kutokana na majeraha ya moto na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliokufa kuwa 21.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment