JUBA, SUDAN KUSINI
PAPA FRANCIS
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni Papa Francis ametoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini kuweka “mwanzo mpya” wa amani nchini humo.
Akiongea Ijumaa alipoanza ziara ya siku tatu katika nchi hiyo iliyozongwa na vita Papa huyo alionya kwamba historia itawahukumu vibaya viongozi hao kwa vitendo vyao.
“Mchakato wa amani na maridhiano unahitaji kuanzishwa upya,” Francis mwenye umri wa miaka 86, akasema kwenye hotuba yake katika Ikulu ya Rais jijini Juba, Sudan Kusini.
Alitaka juhudi kabambe ziendeshwe kukomesha kabisa katika taifa hilo changa zaidi duniani.
“Vizazi vijavyo, ama vitatukuza majina yenu au kuyafuta katika kumbukumbu zao, kwa misingi ya yale mnafanya sasa,” akaambia hadhira iliyowaleta pamoja Rais Salva Kiir, Naibu wake wa kwanza Riek Machar, wanadiplomasia, viongozi wa kidini na wafalme wa kitamaduni miongoni mwa watu wengine.
Tangu Sudan Kusini ilipotangazwa kuwa huru kutoka Sudan mnamo 2011, amani haijashuhudiwa katika nchi hiyo inayozongwa na umaskini.
Mwa miaka mitano, wanajeshi waaminifu kwa Kiir na wale ambao ni watiifu kwa Machar wamekuwa wakipigana. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu 380,000 na wengine milioni nne wakafurushwa makwao.
“Mkomeshe umwagaji damu, mkomeshe vita na hali ya kulaumiana kuhusu ni nani mhusika. Msiwaache watu wenu na kiu ya amani. Wanataka amani haraka,” Francis akasema.
Ziara hiyo ya amani ni ya kwanza kwa Papa kufanya nchini Sudan Kusini tangu nchi hiyo – ambako raia wengi ni Wakristo – kupata uhuru kutoka Sudan yenye idadi kubwa ya Waislamu.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alitua nchini baada ya kufanya ziara ya siku nne katika nchini ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Vita vimechacha mashariki mwa nchini hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini.
Watu wengi, ambao walipiga foleni katika barabara za Jubaa kwa saa kadhaa kubla ya Papa kuwasili, walishangilia msafara wake uliopitia barabara zilizowekwa lami juzi.
Watu wengine walipiga magoti alipopita akiwapungia mkono.
Wengine walivalia mavazi ya kitamaduni au mavazi ya kidini, huku wengine wakipiga firimbi, kupuliza pembe na kuimba nyimbo za kikristo.
Kando na viongozi wa kisiasa, Papa Francis pia anatarajiwa kukutana na waathiriwa wa mapigano, viongozi wa makanisa na kuongoza ibada kubwa leo. Watu wengi wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo.
Ziara hiyo ya Papa, ya tano barani Afrika, ilikuwa imepangiwa kufanyika 2022 lakini ikaahirishwa kwa baada ya Kiongozi huyo kukumbwa na tatizo la goti.
Tatizo hilo limefanya kutembea kwa kutumia viti vya magurudumu.
Mnamo 2019, Francis alitoa ahadi ya kuzuru Sudan Kusini alipokutana na Rais Kiir na Dkt Machar waliomtembea jijini Vatican. Aliwataka kuheshimu mkataba wa amani kwa manufaa ya raia wao.
No comments:
Post a Comment